Utangulizi
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii
inapenda kutoa taarifa kwa umma juu ya kuwepo kwa ugonjwa wa homa ya
dengue yaani “dengue fever” hapa nchini. Ugonjwa huu umethibitishwa
baada ya sampuli zilizochukuliwa kutoka kwa watu waliohisiwa kuwa na
ugonjwa huu jijini Dar es salaam kupelekwa kwenye maabara yetu ya Taifa
Dar es salaam na kuthibitisha kuwa na virusi vya homa ya dengue mnamo
mwishoni mwa mwezi wa Januari. Hadi sasa idadi ya wagonjwa ambao
wamethibitishwa kuwa na ugonjwa huu ni 21 na hakuna mgonjwa yeyote
aliyepoteza maisha.
Homa ya Dengue
Homa ya dengue ni ugonjwa unaosababishwa na kirusi ambacho kinaenezwa na mbu wa aina ya Aedes.
Dalili za ugonjwa huu ni homa,
kuumwa kichwa, maumivu ya viungo na uchovu. Dalili hizi huanza
kujitokeza kuanzia kati siku ya 3 na 14 tangu mtu alipoambukizwa kirusi
cha homa ya dengue. Wakati mwingine dalili za ugonjwa huu zinaweza
kufanana sana na dalili za malaria, hivyo basi wananchi wanaombwa kuwa
wakati wakipata homa kuhakikisha wanapima ili kugundua kama wana vimelea
vya malaria ua la ili hatua stahiki zichukuliwe.
Virusi vya homa ya dengue
vinaenezwa kwa binadamu baada ya kuumwa na mbu aina ya “Aedes”. Mbu
hawa hupendelea kuzaliana kwenye maji yaliyotuama karibu na makazi ya
watu au hata ndani ya nyumba. Viluwiluwi vya mbu hawa huweza kuishi
katika mazingara ya ndani ya nyumba mpaka wakawa mbu kamili na kuanza
kusambaza ugonjwa huu kwa binadamu. Mbu hawa huwa na tabia ya kuuma
wakati wa mchana.
Ugonjwa huu hauenezwi kutoka kwa binadamu mmoja kwenda kwa
mwingine. Homa ya dengue inaweza kutibika kama mgonjwa atapelekwa
hospitali mapema na kupatiwa matibabu ya haraka. Hakuna tiba maalumu ya
ugonjwa wala chanjo bali mgonjwa anatibiwa kutokana na dalili
zitakazoambatana na ugonjwa huu kama vile homa, kupungukiwa maji au
damu. Endapo mgonjwa atachelewa kupatiwa matibabu, mgonjwa anaweza
kupoteza maisha.
Jinsi ya kujikinga na ugonjwa wa homa ya dengue
o Kuangamiza mazalio ya mbu
Fukia madimbwi ya maji yaliyotuama au nyunyuzia dawa ya kuua viluwiluwi vya mbu kwenye madimbwi hayo
Ondoa vitu vyote vinavyoweza kuweka mazalio ya mbu kama
vile, vifuu vya nazi, makopo, magurudumu ya magari yaliyotupwa hovyo,
nk.
Fyeka vichaka vilivyo karibu na makazi ya watu
Hakikisha maua yandayopandwa kwenye makopo au ndoo hayaruhusu maji kutuama
Funika mashimo ya maji taka kwa mfuniko imara
Safisha gata za paa la nyumba ili kutoruhusu maji kutuama
o Kujikinga na kuumwa na mbu
Tumia dawa za kufukuza mbu “mosquito repellants”
Vaa nguo ndefu kujikinga na kuumwa na mbu
Tumia vyandarua vyenye viuatilifu (hata kwa wale wanaolala majira ya mchana)
Weka nyavu kwenye madirisha na milango ya nyumba za kuishi
Hatua zinazochukuliwa na Wizara
• Kutoa taarifa ya tahadhari
ya ugonjwa kwa Waganga Wakuu wote wa Mikoa na Wilaya kwa Tanzania Bara
kupitia Makatibu Tawala na Wakurugenzi.
• Kuimarisha ufuatiliaji wa ugonjwa huu kupitia kwa
Wataalamu wa Afya katika Mikoa, Wilaya na maeneo ya mipakani. Aidha
uchunguzi wa ugonjwa huu utafanyika kwenye Mikoa na Wilaya
zitakazoonekana kuwa na ongezeko la wagonjwa wenye homa.
• Kutuma vipeperushi vya
ugonjwa huu katika maeneo ya mipakani ili iwapo msafiri anayeondoka au
kurudi nchini akiwa na dalili tajwa atoe taarifa kwa watumishi wa afya
wa mpakani ili hatua stahili ziweze kuchukuliwa.
• Kutoa mafunzo kwa
watumishi wa afya na mipakani wa namna ya kutambua na kujikinga dhidi
ya maambukizo ya ugonjwa huu pamoja na uchukuaji wa sampuli iwapo
mgonjwa atapatikana.
• Kuimarisha ufuatiliaji wa
magonjwa nchi nzima kwa kutumia mfumo uliopo wa ukusanyaji wa taarifa,
ambapo tunaendelea kupata taarifa za kila siku juu ya mwenendo wa
ugonjwa huu
• Kuimarisha mfumo wa ufuatiliaji wa ugonjwa wa dengue uliopo kwenye vituo maalumu ‘Sentinel Surveillance Sites’
• Kuimarisha Utambuzi wa ugonjwa katika maabara ili kuweza kuthibitisha ugonjwa huu
• Kufanya tathmini ya
mazalio ya mbu ili kubaini ukubwa wa tatizo, jamii ya mbu wanaoambukiza
ugonjwa, mazingira yao na jinsi ya kuwathibiti
Hitimisho
Wananchi wanashauriwa kutokuwa na hofu kuhusu ugonjwa huu bali wanashauriwa kwenda katika vituo vya tiba mara mnapoona dalili.
Ugonjwa huu si mpya. Mara ya
kwanza kugundulika kuwepo kwa ugonjwa huu nchini ilikuwa ni Juni 2010
mkoani Dar es salaam ambapo idadi ya watu waliothibika kuwa na ugonjwa
ilikuwa 40, pia kati ya mwezi Mei hadi Julai 2013, wagonjwa 172
walithibitishwa kuwa na ugonjwa huu. Hakuna mgonjwa yeyote aliyepoteza
maisha.
Wizara inasisitiza kuwa hakuna vikwazo vyovyote vilivyowekwa kwa
ajili ya wasafiri wanaoingia na wanaotoka nchini. Wizara itaendelea
kushirikiana na sekta mbalimbali kufuatilia na kudhibiti ugonjwa huu.
No comments:
Post a Comment