Moja kati ya sababu inayochangia
wanafunzi wa shule za msingi kumaliza shule bila kujua kusoma na
kuandika inatokana na kukosa mwongozo kuanzia ngazi ya familia kushindwa
kuwanunulia vitabu vya kujisomea.
Ni kwamba familia nyingi hazina
utamaduni wa kusoma vitabu, hali ambayo inasababisha pia kutowashawishi
hata watoto wao kusoma vitabu.Idadi ya watu wasiojua kusoma na kuandika
Ripoti ya Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco) inasema watu wasiojua kusoma na kuandika Duniani wamefikia 774 milioni .
Ripoti hiyo inaeleza wazi kuwa idadi kubwa ya watu hao wasiojua kusoma na kuandika wengi wao wanaishi katika bara ya Afrika na Asia, na kwamba takwimu hizo zinaonyesha kiwango hicho kimeongezeka wa asilimia nane kuanzia mwaka 1990.
Kwa upande wa Tanzania hadi kufikia mwaka 2002 idadi ya watu wasiojua kusoma na kuandika ilikuwa watu 6.2 milioni. Idadi hiyo ni kwa watu wenye umri wa miaka 15 na kuendelea ambao ni sawa na asilimia 31, lakini kwa sasa idadi hiyo imeongezeka na kufikia watu zaidi ya milioni 14.
Mtaalamu wa Masuala ya Elimu kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT) John Masanja, anasema zaidi ya watu 14milioni hawajua kusoma na kuandika hapa nchini na kwamba idadi hiyo inasababisha washindwe kujitambua na kujishughulisha, hivyo kusababisha umasikini .
Masanja anasema Serikali ina wajibu wa kuboresha mifumo yake ya utoaji wa elimu, kwani bila kufanya hivyo kuna uwezekano wa kurudi nyuma kimaendeleo na kiuchumi kutokana kuendelea kuwa na watu wasiojua kusoma wala kuandika. Kutokana na tatizo hilo, Mradi wa Vitabu vya Watoto nchini uitwao Children Books Project (CBP) umeanzisha progamu ya usomaji wa vitabu katika shule za msingi 196 zilizopo katika wilaya 14.
Lengo la kuanzishwa kwa mradi huo ni kujenga utamaduni wa kusoma kwa watoto wa shule za msingi kwa kuwapatia mafunzo na vitabu bora vya kujisomea.
Mratibu wa Mafunzo na Ufuatiliaji kutoka CBP, Marcus Mbigili anasema tathmini ya watoto wa shule za msingi inaonyesha kuwa watoto wengi hawana uwezo wa kutosha wa kusoma.
Anasema Mradi wa Vitabu vya Watoto ulianzishwa mwaka 1991 kutokana na hali mbaya iliyokuwepo ya ukosefu wa vitabu vya kujisomea hasa vitabu vya watoto.
Mbigili anasema katika awamu ya kwanza ya mradi huo, kazi kubwa ilikuwa kushirikiana na wachapishaji kuchapa vitabu vya watoto huku awamu ya pili ilikuwa na malengo ya kushirikiana na wachapishaji kuchapa vitabu, kushirikiana na walimu, kuboresha ujuzi wa kusoma na kuimarisha wadau wa tasnia ya vitabu.
Mratibu huyo anafafanua kuwa katika awamu ya pili, pamoja na kuwepo idadi kubwa ya vitabu vya watoto, bado kulikuwa na matatizo ya kusoma miongoni mwa wanafunzi katika shule mbalimbali hapa nchini.
"Kutokana na matatizo haya, mradi wa CBP ulizindua programu ya usomaji wa vitabu kwa baadhi ya shule za msingi kwa lengo la kumfanya mtoto asome kwa maana ya kupata maarifa, ufahamu na burudani"anasema Mbigili.
"Programu hii ilianza kwa majaribio katika shule sita za Mkoa wa Dar es Salaam na sita kwa Mkoa wa Pwani na kazi kubwa ilikuwa ni kutoa mafunzo kwa walimu wa shule hizo mbinu za kufundishia, uanzishwaji wa maktaba, uandaaji wa vitabu na zana za kufundishia,"anaongeza.
Shule zilizopo katika mradi huo wa CBP
Mpaka sasa jumla ya shule 196 kutoka wilaya 14 za hapa nchini zimeunganishwa katika mradi wa huo na kwamba wilaya hizo ni Kinondoni, Ilala, Temeke, Mkuranga, Bagamoyo, Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha, Halmashauri ya Mji wa Kibaha, Morogoro Mjini na Morogoro Vijijini, Kilosa, Kisarawe, Rufiji, Mvomero na Kongwa mkoani Dodoma. Chanzo: mwananchi
No comments:
Post a Comment